MTUHUMIWA wa wizi wa Sh 7 milioni kwa kila dakika Mohammedi Mustafa na mwenzake, wamepandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kesi nyengine ya kuhujumu uchumi, anaandika Faki Sosi.
Katika kesi ya sasa, mtuhumiwa namba moja ni Sammuel Lema, Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Work Limited huku Mohamed akiwa ni mtuhumiwa namba mbili ambapo wamesomewa jumla ya mashitaka 222.Akisoma mashitaka yao Kishenyi Mutalemwa wakili wa Serikali mbele ya Wilbard Mashauri hakimu mkazi mahakama ya Kisutu katika kesi Na. 36 ya 2016, amesema watuhumiwa hao walipanga njama za kufanya makosa kati ya tarehe 1 Februari mwaka 2013 hadi 31 Disemba 2015.
Kishenyi amedai kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda makosa ya kughushi nyaraka mbalimbali za mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kuanzia kosa Na. mbili hadi kosa Na. 103 huku kosa Na. 104 hadi 142 yakidaiwa kufanywa na mtuhumiwa namba moja pekee.
Keshinyi amedai kuwa shitaka la 220 ambalo ni la kukwepa kulipa kodi lilifanywa kati ya 1 Februali 2013 hadi 13 Desemba 2015 ambapo mshitakiwa namba moja katika shauri hilo anatuhumiwa kukwepa kodi yenye thamani ya Sh.14 bilioni.
Shitaka la 221 linalohusu utakatishaji fedha linadaiwa kutendwa na washitakiwa wote wawili kati ya 1 Februali 2013 na 31 Disemba 2015 ambao inadaiwa kiasi cha fedha Sh. 400 milioni zilitakatishwa kupitia akaunti ya Iqbal Jafareri katika Benki ya IMM tawi la Kariakoo.
Shitaka la mwisho ni kuisababishia TRA hasara ya Sh 13 bilioni kwa ukwepaji kodi. Kutokana na mashtaka hayo watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mahakama ya hakimu mkazi wa Kisutu kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza.
Alex Mgongolwa wakili wa upande wa utetezi baada ya wateja wake kusomewa mashitaka aliwasilisha hoja za kupinga shitaka Na. 221 linalohusu utakatishaji fedha akidai lina upungufu kisheria ambao hauwezi kurekebishika na kwamba maelezo ya shitaka hilo hayajitoshelezi.
Kishenyi wakili wa upande wa serikali ameiomba Mahakama kuwapa muda wa siku mbili ili kuweza kujibu hoja za upande wa utetezi.
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka 28 Julai mwaka huu, itakumbukwa kuwa mtuhumiwa namba mbili Mohamed Mustafa anakabiliwa na kesi nyingine kama hiyo katika mahakama ya hakimu mkazi wa Kisutu ambapo alisomewa jumla ya mshitaka 199.
Post a Comment